Mashahidi wa Ruto katika ICC

Mashahidi wa kwanza kwenye kesi inayowakabili watuhumiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya wamefika mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC , mjini The Hgaue leo.

Haki miliki ya picha Christian Science Monitor

Mashahidi hao ni wa upande wa mmoja wa watuhumiwa - Bwana William Ruto, aliyekuwa waziri wa elimu ya juu.

Shahidi wa kwanza kupanda kizimbani amekuwa Samson Cheramboss, ambaye ni mkuu wa zamani wa kikosi maalum cha Polisi cha kupambana na ghasia nchini Kenya.

Yuko mahakamani kama shahidi wa kujibu tuhuma za mahakama kwamba Bwana Ruto alifanya mikutano kadhaa ya kuandaa mashambulizi dhidi ya watu kutoka jamii zilizoonekana kuunga mkono chama cha Rais Kibaki cha PNU.

Upande wa mashtaka hapo jana ulimtaja shahidi huyo miongoni mwa maafisa wakuu wa jeshi wastaafu wanaodaiwa kuagizwa na Bwana Ruto kuongoza mashambulizi hayo.

Amekanusha kuwepo kwa mikutano ya aina hiyo.

Shahidi mwingine aliyehojiwa ni Andrew Kiprono Murray, kwa jina lingine Kabarosna, na yeye ni jirani wa Bwana Ruto, na pia mwenyekiti wa kamati ya amani ya eneo la Eldoret mashariki.

Ameelezea mahakama namna walivyojaribu kuwaokoa watu wa makabila bila msaada wowote kutoka Polisi.