Urusi inalaani vikwazo dhidi ya Syria

Wakati vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya mafuta kutoka Syria vinaanza kutekelezwa, Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amelaani vikwazo hivo.

Serikali za nchi za Umoja wa Ulaya zilikubaliana Ijumaa kuzidisha vikwazo kwa sababu ya hatua kali zinazochukuliwa na Syria, kukandamiza maandamano dhidi ya serikali.

Umoja wa Ulaya umepiga marufuku mafuta kutoka Syria, ingawa kandarasi zilioko hivi sasa zinaweza kuendelea hadi Novemba.

Bwana Lavrov alisema vikwazo hivo havitaleta manufaa, na vitachafua juhudi za kimataifa za kushirikiana ili kushughulikia msukusuko wa Syria.

Katika fujo za hivi karibuni kabisa, wanaharakati wa Syria wamesema watu kama 17 waliuwawa Ijumaa katika mandamano dhidi ya Rais Bashar Al-Assad.