Eritrea inakabili njaa piya

Ukame na njaa iliyokumba pembe ya Afrika inaathiri watu zaidi ya milioni 12.

Lakini nchi moja katika eneo hilo, Eritrea, inasema kuwa imevuna mazao mengi mwaka huu.

Hata hivo, ushahidi unaonesha kuwa hali halisi ni tofauti katika nchi hiyo inayoweka mambo yake siri.

Katika mwongo uliopita Eritrea imekuwa moja kati ya nchi iliyojitenga kabisa na ulimwengu; isiyokuwa na vyombo vya habari huru wala upinzani.

Kwa hivo ni shida kuthibitisha matamshi ya serikali kwamba watu wa nchi hiyo wana chakula cha kutosha.

Lakini sasa, picha tofauti inajitokeza: kwamba thuluthi mbili ya WaEritrea wana njaa.

Picha za satalaiti zinaonesha mvua iliyonyesha wakati wa masika, baina ya Juni na Septemba, ilikuwa haba.

Na miaka iliyopita kulikuwa na ukame.

Athari kwa wananchi inaonekana kaskazini mwa Ethiopia, ambako waEritrea waliokonda na kudhoofika kwa njaa, wanavuka mpaka wenye ulinzi mkubwa.

WaEritrea 900 wanakimbilia Ethiopia kila mwezi; na wanaeleza kuwa mazao yamekauka na chakula hamna majumbani.

Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice, amesema ilivoelekea ni kuwa watu wa Eritrea wanakabili njaa kama wengine katika kanda hiyo, lakini wanaachwa kutapia mlo kwa sababu haiwezekani kuwafikia.