Sudan Kusini yataka mji mkuu mpya

Taifa jipya kabisa duniani, jamhuri ya Sudan Kusini, imeamua kuhamisha mji mkuu wake.

Haki miliki ya picha AP

Mji mkuu wa sasa ni Juba lakini pahala pengine pamechaguliwa kati ya nchi.

Sudan Kusini ilipata uhuru mwezi July, baada ya vita vya mwongo kadha.

Baada ya majadiliano ya miezi kadha, sasa imeamuwa kuwa mji mkuu wa Sudan Kusini utahamishiwa Ramciel.

Ramciel iko kati-kati ya nchi, kwenye jimbo la Lakes, lakini karibu na majimbo kadha mengine.

Taarifa moja inaelezea eneo hilo kuwa ni mbali, hakujajengwa, na hakuna miundo mbinu.

Serikali inakiri kuwa itachukua miaka kadha kujenga mji mkuu mpya, na serikali itahamia huko kwa awamu.

Sababu moja ya kuchukua uamuzi huo, ni kwa sababu kabila la Bari, lilioko Juba na maeneo ya karibu, inasemekana limeomba mji mkuu uhamishwe.

Kabila la Bari lina wasiwasi kuwa ardhi yake inachukuliwa na serikali.

Kuna ugomvi mara kadha kuhusu ardhi Juba na kwengineko kusini mwa Sudan.

Swala la wapi kujenga mji mkuu ni nyeti, katika nchi yenye makabila mengi.

Lakini pahala pepya ni karibu na shina la kabila la WaDinka, kabila kubwa kabisa la Sudan Kusini, ambayo inaweza kuzusha chuki kati ya WaSudan Kusini.

Baraza la mawaziri limesema mjadala kuhusu wapi kujenga mji mkuu umeendelea kwa muda mrefu, na imezuwia maendeleo Sudan Kusini tangu mwaka wa 2005, wakati eneo hilo lilipopata uhuru wa kadiri fulani.