Kosgey aamua kutowaita mashahidi

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita iliyoko mjini The Hague, Uholanzi, inaendelea na utaratibu wa kuhakiki ikiwa kuna ushaidi wa kutosha wa kuwashtaki watuhumiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya, mwaka 2007.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Henry Kosgey aliamua ghafula kutowaita mashahidi

Jumatatu mashahidi wa mshukiwa wa pili, Henry Kosgey, ndio waliotarajiwa kuhojiwa.

Mwandishi wa BBC huko The Hague, Peter Musembi, anaelezea kwamba Bw Henry Kosgey alifanya uamuzi wa dakika ya mwisho wa kutoleta shahidi yeyote mbele ya mahakama kama ilivyotarajiwa.

Badala yake, wakili wa Bwana Kosgey, George Oraro, amechukua fursa kutoa pingamizi zake kuhusu ushahidi dhidi ya Kosgey, uliowasilishwa na kiongozi mkuu wa mashtaka Luis Moreno Ocampo.

Bwana Ocampo anamtuhumu mwenyekiti huyo wa chama cha ODM kwa madai ya kufadhili mtandao unaosemekana uliendesha mashambulizi ya kuuwa na kufukuza watu wa jamii zilizounga mkono chama cha Rais Kibaki cha PNU mkoani Rift Valley.

Wakili huyo ameelezea mahakama kuwa Bw Kosgey hakutoa mwongozo au kufadhili kundi kama hilo, na kwamba hakushiriki mikutano yoyote inayodaiwa kupangwa ili kuendesha mashambulizi.

Tayari mashahidi wa Bw Ruto, mbunge wa Eldoret ya Kaskazini nchini Kenya, wameshahojiwa, na wakakanusha kufanyika mikutano yoyote nyumbani kwa Ruto kuandaa mashambulizi.

Mashahidi wa mshukiwa wa tatu , mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang, wanatazamiwa kufika mahakamani Jumanne.

Sang anatuhumiwa kwa kutumia vipindi vya redio kusaidia mashambulizi hayo.