Ghasia wakati kesi ya Mubarak ikianza

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bw Hosni Mubarak kwenye machela

Purukushani zimeibuka baada ya kesi ya aliyekuwa Rais Hosni Mubarak kuanza upya kwenye mji mkuu wa Misri, Cairo.

Polisi wa kuzuia ghasia walikuwa wakitenganisha mkusanyiko wa waandamanaji wanaompinga na wanoamwuunga mkono nje ya mahakama kwenye chuo cha mafunzo cha polisi ambapo kesi hiyo inasikilizwa.

Bw Mubarak mwenye umri wa miaka 83 anatuhumiwa kwa kuamuru mauaji ya waandamanaji wakati wa machafuko mapema mwaka huu yaliyomaliza utawala wake.

Amekana mashtaka hayo.

Hii ni mara ya tatu tangu kesi hiyo kuanza kusikilizwa. Jaji amezuia kesi hiyo kuonyeshwa kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni.

Picha kupitia televisheni zilimwonyesha kiongozi huyo wa Misri aliyeshika madaraka kwa miaka 30 akiwa kwenye kizimba cha vyuma katika machela kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa siku ya kwanza ambapo watu kutoka nchi za kiarabu walilazimika kutazama.

Maofisa wanne wa polisi, akiwemo afisa mwandamizi, walioshiriki katika harakati hizo wakati huo wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo siku ya Jumatatu.

Hisia zilipamba moto nje ya mahakama, iliyopo nje ya Cairo, aliripoti mwandishi wa BBC Bethany Bell aliyekuwepo eneo la tukio.

Wengine walishangilia wakimwuunga mkono Bw Mubarak huku wengine wakisema anyongwe.