Kesi ya Ingabire yaamuriwa kuanza Rwanda

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bi Victoire Ingabire na wakili wake Iain Edwards

Jaji wa Rwanda ameamuru kesi inayomkabili kiongozi wa upinzani Victoire Ingabire iendelee.

Anatuhumiwa kwa kueneza propaganda za chuki za kikabila na " kukana kutokea kwa mauaji ya kimbari"- mashtaka anayosema yamechochewa kisiasa.

Upande wa mashtaka ulitaka kesi hiyo iahirishwe mpaka ushahidi zaidi uwasilishwe kutoka Uholanzi, ambapo Bi Ingabire aliishi mpaka Januari 2010.

Alikamatwa mwezi Aprili na kuzuiwa kugombea katika uchaguzi wa mwaka jana.

Alifikishwa mahakamani akiwa na pingu, na kuvaa sare ya Rwanda ya gerezani kama ilivyo ada ya rangi ya waridi huku akiwa amekatwa kipara.

Mwandishi wa BBC Geoffrey Mutagoma aliyopo mjini Kigali alisema ni kawaida kwa wafungwa wa Rwanda kukatwa kipara kutokana na sababu za kiafya.

Wakili wake wa Uingereza Iain Edwards alitaka kesi hiyo ianze kusikilizwa kama ilivyokuwa imepangwa na Jaji Alice Rulisa akakubali.

"Mwendesha mashtaka alisema tangu mwanzo kwamba wako tayari kwa kesi hiyo kuanza kusikilizwa, na wana ushahidi wote wa kuweza kuanza kesi hiyo," alisema.

"Sasa wanasema wanahitaji muda zaidi."

Kesi hiyo ishacheleweshwa katika vipindi viwili tofauti.

Kiongozi huyo wa chama cha Unified Democratic Forces anatuhumiwa kwa kula njama na aliyekuwa afisa wa jeshi la Kihutu wa kununua na kusambaza silaha za kutishia usalama wa taifa.

Bi Ingabire alisema mashtaka hayo si ya kweli na yamechochewa kisiasa.

Mwandishi wetu amesema ikiwa atakutwa na hatia, huenda akapewa kifungo cha maisha.

Bi Ingabire ni Mhutu na wengi miongoni mwa 800,000 waliouawa kwenye ghasia za mwaka 1994 walikuwa ni Watutsi.

Rais Paul Kagame, aliyekuwa kiongozi wa waasi wa chama cha Rwandan Patriotic Front (RPF) chenye Watutsi wengi alisitisha mauaji hayo ya kimbari, alishinda kwa kipindi cha pili cha urais Agosti 2010 kwa jumla ya asilimia 93 ya kura zote.