Uefa wazidi kumbana Arsene Wenger

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger rufaa yake ya kuzuiwa na Uefa kukaa katika benchi la ufundi la timu hiyo katika mechi za Ubingwa wa Ulaya imegonga mwamba.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Arsene Wenger

Wenger aliadhibiwa baada ya kupatikana na hatia ya kuwasiliana na benchi la ufundi la Arsenal wakati akitumikia adhabu ya kukaa kwenye benchi la ufundi mwezi wa Agosti wakati timu yake ilipoilaza Udinese bao 1-0.

Arsenal pia imepigwa faini ya euro 10,000 sawa na paundi 8,700 kutokana na utovu wa nidhamu.

Wenger sasa ataiangalia timu yake akiwa jukwaa la watazamaji kwa mechi za makundi mwezi wa Septemba dhidi ya Borussia Dortmund na Olympiakos.

Meneja huyo wa The Gunners aliaamini hakufanya kosa baada ya klabu kumwambia anaweza kutuma ujumbe kwa msaidizi wake Pat Rice kupitia kwa kocha katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Arsenal ya kufuzu dhidi ya Udinese katika uwanja wa Emirates. Wakati huo aliambiwa wakati wa mapumziko hakuwa ameruhusiwa kufanya hivyo.

Wenger baadae alisema inakera kwa vile klabu iliiuliza Uefa kabla ya mechi kwa ajili ya ufafanuzi wa kanuni na yeye alikuwa anazifuata.

Klabu ya Arsenal ilikata rufaa dhidi ya adhabu hiyo na Uefa ikaafiki kuweka kando uamuzi wake hadi baada ya mechi ya pili ya marudiano ambapo Arsenal ilifanikiwa kusonga mbele katika hatua ya makundi.