Capello akiri England walikuwa na bahati

Fabio Capello amekiri England ilikuwa na bahati kushinda dhidi ya Wales matokeo yaliyoiweka katika nafasi ya kufuzu kwa mashindano ya nchi za Ulaya yaitwayo Euro fainali zake zitakazofanyika mwaka 2012 na akadai wachezaji wake wanakuwa hawajiamini wanapocheza katika uwanja wa Wembley.

Image caption Fabio Capello

Bao la Ashley Young katika dakika ya 35 limeipa England ushindi wa kwanza katika uwanja wa Wembley kwa zaidi ya mwaka mmoja na sasa wanahitaji pointi moja tu katika mchezo wao wa mwisho watakapokumbana na Montenegro mwezi ujao ili iweze kusonga mbele katika fainali zitakazochezwa Poland na Ukraine.

Lakini ulikuwa mchezo wa kiwango cha chini uliooneshwa na wachezaji wa England na walikuwa na bahati kwani wangeweza kupoteza pointi zote tatu baada ya Robert Earnshaw aliyeingizwa mchezaji wa akiba wa Wales, mkwaju wake wa karibu na lango ulipaa juu zikiwa zimesalia dakika 13 kabla mchezo kumalizika.

Capello alisema: "Tulikuwa na bahati. Wakati mchezaji wao alipofanya makosa makubwa mbele ya lango ilikuwa bahati kwetu, lakini naona hatukucheza vizuri sana katika dakika 15 za mwisho na tulikuwa tunahaha.

"Tulicheza vizuri sana kwa dakika 20 kipindi cha kwanza, lakini tunahitajika kucheza vyema kwa muda wote wa mchezo."