Kesi ya Hosni Mubarak Misri

Hosni Mubarak Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Hosni Mubarak

Kesi ya aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak inafanyika katika mji mkuu wa Cairo.

Iliahirishwa kwa siku moja baada ya vurugu kuzuka mahakamani Jumatatu kati ya wafuasi wake na wale wa upinzani.

Mubarak mwenye umri wa miaka 83 anashtakiwa kwa kuamuru kuuawa kwa waandamanaji wakati wa harakati za kutaka mageuzi mapema mwaka huu zilizomaliza utawala wake.Anakunusha madai yote.

Mmoja kati ya mashahidi wa kwanza amekanusha kuwa waziri wa mashauri ya ndani wa Mubarak alitoa maagizo kuwa waandamanaji wapigwe risasi.

Siku ya Jumatatu, upande wa mashtaka uliwataka maafisa wanne wa Polisi katika ngazi za juu watoe ushahidi kuhusu wajibu uliotekelezwa na Mubarak katika kuzima maandamano hayo.

Jenerali Hussein Saeed Mohamed Mursi, mmoja wa maafisa hao kutoa ushahidi siku ya Jumatatu, aliiambia mahakama kuwa Polisi waliagizwa wawazuie waandamanaji kufika katika uwanja wa Tahrir na kutokana na matukio waliwajibika kuchukuwa hatua walizoona zinafaa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuter Jenerali Hussein alisema hakupata kusikia wakiagizwa watumie risasi za moto dhidi ya waandamanaji.

Watu walipandwa na mori nje ya mahakama wakati wa kusikizwa kesi hiyo siku ya Jumatatu, ambapo baadhi ya watu waliimba nyimbo za kumsifu ilhali wengine wakisema anapaswa kunyongwa.

Kulikuwa na vurugu hata ndani ya mahakama, mtu mmoja aliinua na kuibeba juu kwa juu picha ya Mubarak ambayo baadae ilichukuliwa na kuteketezwa.

Katika utaratibu wa usikizwaji wa kesi hii hapo awali, picha za televisheni zilimuonesha Bw Mubaraka, ambaye aliongoza Misri kwa miaka 30 akiwa katika kitanda cha wagonjwa kwenye kizimba kilichozungushwa vyuma.Lakini Jaji anaeendesha kesi hii aliamua kupiga marufuku shuguhuli za kesi hiyo kuonekana moja kwa moja katika televisheni.