8 Septemba, 2011 - Imetolewa 11:17 GMT

Mutola aibukia katika soka

Media Player

Unahitaji toleo sahihi la Flash Player kucheza sauti/video

Cheza katika media player


Wakati Maria Mutola alipomaliza katika nafasi ya tano kwenye fainali ya mbio za mita 800 katika michuano ya Olimpiki mjini Beijing, akiwa na umri wa miaka 35, ilionekana huo ndio mwisho wa Maria, maarufu kama "Maputo Express".

Lakini miaka mitatu baada ya kustaafu mchezo wa riadha, Mutola ameibuka na safari hii ni mcheza soka na ni nahodha wa timu ya taifa ya wanawake ya Msumbiji katika michuano ya Afrika inayofanyika mjini Maputo.

Mutola

Maria Mutola

Kuibuka kwake kunakamilisha mzunguko wa fani yake katika michezo ambayo imeshuhudia akishinda medali ya dhahabu katika Olimpiki na mataji 10 ya dunia. Mutola alishawishiwa kuingia katika riadha zamani baada ya kuonekana akicheza soka na watoto wa kiume katika mitaa ya Maputo.

Kwa sasa anaishi jijini Johannesburg, Afrika Kusini ambapo huichezea timu ya soka ya wanawake ya Mamelodi Sundowns ya Pretoria.

Mutola ameiambia BBC: "Ilikuja kwa kunishtukiza tu - rafiki yangu mmoja alikuwa akicheza Afrika Kusini aliniomba niende kumsaidia kidogo.

"Halafu wakaona bado ninaweza kucheza, wakaniomba nicheze na mimi nikaamua kujaribu, na nikaona nafurahia.

"Ni kama kurudi nyumbani - najua jinsi ya kucheza soka, nilihitaji mazoezi kidogo, na nimekuwa nikifanya hivyo, kwa hiyo nadhani mambo yanakaa vizuri kwa sasa."

Katika fani ya riadha, Mutola ameshinda zaidi ya mataji 10 ya dunia, ya viwanja vya ndani na nje na medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki iliyofanyika Sydney mwaka 2000.

Kwa kuwa nchi yake ndio mwenyeji wa michuano ya Afrika, fani hii mpya ya Mutola imempa nafasi isiyo ya kawaida kushiriki katika michuano mikubwa kuwahi kufanyika nchini Msumbiji.

Timu ya soka ya wanawake ya Msumbiji imefuzu kucheza michuano hiyo kwa sababu ni nchi waandaaji, lakini ndio timu dhaifu zaidi kati ya timu nane zinazoshiriki, ikiwa na wachezaji wengi vijana na wasio na uzoefu katika timu ambayo imeundwa miezi michache iliyopita.

Mutola, akicheza kama mshambuliaji, alionesha ufundi mkubwa wa kusakata kandanda katika mchezo wa kwanza wa Msumbiji dhidi ya Cameroon. Ingawa Mamba hao wa msumbiji walifungwa 1-0, walikuwa na bahati ya kuondoka uwanjani bila kufungwa mabao mengi.

Kwa hiyo nafasi ya Mutola na wachezaji wenzake kupata medali katika michuano hii ni finyu, lakini utakuwa ukurasa mwingine wa kumbukumbu kwa mkimbiaji huyo wa Msumbiji.

Mutola alisema: "Niliitwa kuja kuisaidia timu hii mpya ya taifa kaika michuano ya Afrika.

"Nilishinda medali tatu katika riadha kwenye michuano iliyopita ya Afrika, na kushirikishwa katika maandalizi ya Msumbiji ni jambo la kufurahisha, ingawa sishiriki kama mkimbiaji.

"Natamani muda ungerudi nyuma kidogo, ili nikimbie kuiwakilisha Msumbiji, lakini niko hapa na nimefurahi kuwa sehemu ya michezo hii.

BBC navigation

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.