Mkuu wa Usalama wa Gaddafi ‘awasili Niamey’

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maafisa usalama Libya

Mkuu wa usalama wa Kanali Gaddafi ni miongoni mwa maafisa kadhaa washirika wakewaliowasili katika mji mkuu wa Niger, Niamey, maafisa wamesema.

Wanasema mkuu huyo, Mansour Daw, aliingia nchini Niger Juamapili akiwa amesafiri kupitia njia ya jangwani karibu na mji wa Agadez.

Wakati huo huo, msafara uliotajwa kuwa na washirika wa karibu wanaomtii Kanali Gaddafi ukiwa na silaha nzito na fedha na dhahabu umeelekea katika mji mkuu wa Niger.

Maafisa wa Niger wanasema haiaminiki iwapo Kanali Gaddafi yuko pamoja nao.

Kamanda mwandamizi wa waasi alisema anaamini Kanali Gaddafi bado yuko Libya, lakini akiondoka kukimbia maeneo ambayo mapigano yanatokea.

"Tumepata taarifa kutoka vyanzo vingi kuwa anajaribu kusogea kusini kuelekea Chad au Niger," Hisham Buhagiar alisema katika mahojiano na shirika la habari la Reuters.

Kiongozi huyo wa zamani wa Libya ameapa kupigana mpaka kufa, hata kama amepoteza udhibiti katika sehemu kubwa ya nchi.