Uteuzi wa Rais Mutharika wakosolewa

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Bingu wa Mutharika

Upinzani wa Malawi umemkosoa Rais Bingu wa Mutahrika kwa kumteua mkewe kwenye baraza la mawaziri na kumpandisha cheo kaka yake.

Siku ya Jumatano, Bw Mutharika alimteua mke wake, Callista, kuwa waziri wa masuala ya wanawake na ukimwi.

Amemhamisha kaka yake, Peter, kutoka wizara ya elimu na kumweka kwenye wizara ya mambo ya nje.

Kubadilisha baraza hilo kumefanyika baada ya watu 19 kuuawa kwenye maandamano ya kuipinga serikali mwezi Julai.

Walioandaa maandamano hayo walimpa muda Bw Mutharika mpaka Septemba 21 awe ameshafanya mabadiliko.

Mkuu wa upinzani wa Malawi Congress Party (MCP), John Tembo, alisema anatia shaka uteuzi wa Bi Mutharika na Peter Mutharika kwenye baraza hilo la mawaziri.

Bw Tembo alisema, " Rais bado anahitaji kujieleza kwanini mke wake na kaka yake wako kwenye baraza la mawaziri kabla ya kuanza kumshutumu kwa kupendelea ndugu."

"Pia amewabakiza mawaziri wengi waliotoka kwenye eneo lake la asili ambalo nalo ni kosa."