Hatujampa hifadhi Gaddafi - Niger

Serikali ya Niger imesema kuwa itaamua jinsi ya kumshughulikia Kanali Muamar Gaddafi iwapo ataingia nchini humo kuomba hifadhi ya kisiasa.

Image caption Kanali Gadaffi

Ripoti kutoka eneo hilo zinasema kuwa maafisa wa vyeo vya juu katika Serikali iliyotimuliwa wamewasili nchini Niger na kuna habari kuwa huenda Kanali Gaddafi akajiunga nao.

Baraza la Kitaifa la Mpito la Libya limetoa wito kwa Serikali ya Niger isimpe hifadhi Kanali Gaddafi.

Mwandishi wa Habari wa BBC nchini Libya anasema kuwa ombi hilo limeweka Niger katika hali ya kutatanisha kwa sababu tayari imetambua serikali ya mpito lakini haiwezi kumfukuza Kanali Gaddafi kwa sababu ya uhusiano wa karibu waliokuwa nao viongozi hao wa Niger.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kiongozi wa Baraza la mpito nchini Libya

Wakati huo huo Kanali Gadafi amepuuza madai kwamba ametorokea nchi jirani ya Niger na kuyataja madai hayo kama uongo na vita vya kiakili.

Matamshi ya Gadaffi yamepeperushwa na kituo kimoja cha televisheni nchini Syria, kilichodai kuwa Gadaffi baado yuko nchini Libya.

Gadafi ameapa kuwashinda wapiganaji wa upinzani wanaoungwa mkono na majeshi ya muungano wa NATO.

Huu ndio ujumbe wake wa kwanza katika kipindi kirefu.

Ripoti zinasema katika muda wa siku 10 zilizopita, maafisa wakuu wa uliokuwa utawala wa gadaffi wamekuwa wakiwasili nchini Niger na kuibua fununu kuwa Kanali Gadaffi huenda akajaribu kujumuika nao.

Baraza la kitaifa la mpito nchini Libya limetoa wito kwa Niger kutompa hifadhi. Serikali ya Niger imesema kwamba itaamua jinsi itakavyomshughulikia Kanali muammar gadaffi ikiwa ataingia nchini humo na kuomba hifadhi.