Feri yazama Zanzibar, 'mamia' wafariki

Mamia ya watu wanahofiwa kufariki dunia baada ya feri kuzama katika pwani ya kisiwa cha Zanzibar nchini Tanzania ikiwa imewabeba zaidi ya watu mia tano.

Haki miliki ya picha 1

Zaidi ya watu arobaini na tatu wameaga dunia katika mkasa huo , mmoja wa mawaziri katika kisiwa hicho kinachojitawala amesema.

Takriban watu 260 wameripotiwa kuokolewa

Feri hiyo MV Spice Islander ilikuwa ikisafiri kati ya kisiwa kikubwa zaidi cha Unguja ikielekea Pemba ambacho pia ni kisiwa cha Zanzibar.

"Hadi kufikia sasa tumeopoa miili 43, lakini tumewaokoa manusura 259," amesema Mohammed Aboud, waziri wa Zanzibar anayehusika na mikasa. Ameongeza kuwa 40 kati ya wale waliookolewa walikuwa na mejeraha mabaya.

Likizo ya Ramadhan

Feri hiyo iliondoka Unguja saa nne usiku na inasemekana kuzama majira ya saa saba usiku.

Shirika la habari la AP limeripoti kwamba feri hiyo ilikuwa imebeba abiria kupita kiasi.

Ilikuwa ikiwarejesha watu waliokuwa likizo ya mwezi mtukufu wa Ramadhan na watoto wengi walikuwa miongoni mwa abiria hao.

Mwandishi wa BBC aliyepo Zanzibar amesema miili mingi imeanza kuelea na kusukumwa pwani na maafisa wanakabiliwa na kibarua kigumu kuushughulikia mkasa huo.

Maafisa wametenga eneo maalum la uokoaji na kutoa wito kwa mataifa mengine ya Afrika kutoa msaada wa vifaa maalum vya uokoaji.