Rais Kagame azuru Ufaransa

Rais Paul Kagame
Image caption Rais Paul Kagame wa Rwanda

Ziara ya rais Kagame inafuatia ziara ya rais Nicolas Sarkozy nchini Rwanda mwaka jana. Pamoja na hayo, serikali ya Rwanda inasema kuwa ziara hii ni katika juhudi za kujaribu kukarabati uhusiano wa nchi hizo mbili.

Mwaka 2006, Rwanda ilivunja uhusiano wake na Ufaransa baada ya uchunguzi wa kisheria uliofanywa na Ufaransa kuonyesha kuwa ni chama cha waasi wa RPF ambacho kilitungua ndege ya rais Habyarimana. Abiria wote katika ndege hiyo wakiwemo marais wawili na Wafaransa watatu waliokuwa wafanyakazi wa ndege hiyo walifariki.

Jaji wa Ufaransa, alitoa hati za kuwakamata maafisa tisa wa jeshi la Rwanda. Hatua hiyo iliikasirisha serikali ya Rwanda ambayo ilitamka kuwa uchunguzi huo ulikuwa na makosa na ulipendelea upande mmoja. Serikali ya Rwanda ilivunja uhusino wake na Ufaransa na kuanzisha uchunguzi wake kuhusu kutunguliwa ndege hiyo. Uchunguzi huo ulikamilika kwa kusema kuwa ndege hiyo ilitunguliwa na Wahutu wa msimamo mkali katika jeshi la Rwanda. Uchunguzi huo pia ulitaja kuwa serikali ya Ufaransa ilichangia katika mauaji ya kimbari ya watu wapatao laki nane.Uchunguzi wa Rwanda ulikuwa kinyume na uchunguzi wa bunge la Ufaransa ulionyesha kuwa serikali ya Ufaransa haikushiriki katika mauaji ya Rwanda.

Rwanda iliotoa orodha ya majina 33 ya maafisa wa serikali na jeshi la Ufaransa ambao ilidai kuwa walichangia katika mauaji hayo. Hatahivyo, Rwanda haikutoka nyaraka za kuwakamata. Serikali ya Ufaransa ilikubali kufanya uchunguzi mpya wa kisheria kuhusu kutunguliwa kwa ndege hiyo na taarifa yake inatarajiwa kutangazwa mwaka huu. Ingawa uhusiano wa kibalozi baina ya Rwanda na Ufaransa ulifufuliwa mwaka 2009, bado kuna masuala magumu ambayo hayajatatuliwa. Miongoni mwa masuala hayo, ni watuhumiwa wa mauaji ya kimbari ambao wako Ufaransa akiwemo mjane wa marehemu rais Habyarimana. Nchini Ufaransa kuna wanaolaumu serikali ya nchi hiyo kuwa inapuuza jinsi ripoti ya serikali ya rwanda ilivyoharibu heshima ya nchi na hali uchunguzi wa Rwanda ulifanywa kwa sababu za kisiasa.