Mancini awataka wachezaji kujibidiisha

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amesema kikosi chake hakina budi kucheza vizuri zaidi licha ya ushindi rahisi walioupata dhidi ya Wigan kwenye uwanja wa Etihad.

Image caption Roberto Mancini

Sergio Aguero alifunga mabao yote matatu peke yake na Carlos Tevez akakosa kufunga mkwaju wa penalti wakati timu hiyo ilipoilaza Wigan mabao 3-0, hali inayowafanya hadi sasa wawe wamefunga mabao 15 katika mechi nne za ligi walizocheza msimu huu.

Lakini Mancini hakufurahishwa kutokana na idadi ya nafasi za kufunga zilizopotezwa na wachezaji wake.

"Tulipata nafasi 15 katika kipindi cha kwanza na tukafunga bao moja tu - hili ni tatizo kwa sababu mchezo unaweza kubadilika wakati wowote," alisema Mancini.

"Wakati mwengine ni vyema kumaliza mchezo katika kipindi cha kwanza. Hatuna budi kubadilika kwa sababu tumeuanza vizuri sana msimu huu lakini msimu ni mrefu.

"Iwapo tunataka kukamilisha msimu wa ligi tukiwa kileleni hatuna budi kubadilika na kucheza vizuri zaidi."

Aguero sasa ana jumla ya mabao sita ya kufunga msimu huu na licha ya Tevez kukosa kufunga mkwaju wa penalti, Mancini alisema anaridhishwa na kiwango cha nahodha huyo wa zamani wa Man City.

Edin Dzeko alipumzishwa katika mechi hiyo dhidi ya Wigan wakati huu City ikijiandaa kwa mchezo wa Ligi ya Ubingwa wa Ulaya siku ya Jumatano dhidi ya Napoli.