Al Ahly yafufua matumaini Ubingwa Afrika

Mabingwa mara sita wa soka barani Afrika Al Ahly ya Misri wamefufua matumaini ya kufika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Ubingwa wa Afrika walipotoka sare ya bao 1-1 na Wydad Casablanca ya Morocco.

Image caption Wachezaji wa Al Ahly

Mshambuliaji wa Misri Mohamed 'Gedo' Nagy alikuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika ya 37 kabla ya Abderahim Benkajjane kusawazisha zikiwa zimesalia dakika mbili kabla ya mapumziko.

Nayo klabu ya Tunisia ya Esperance imekalia kiti cha uongozi kundi B baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Mouloudia Alger ya Algeria.

Image caption Wachezaji wa Esperance ya Tunisia

Kwa matokeo hayo ni Mouloudia tu wanaoweza kufika hatua ya timu nne za mwisho za nusu fainali kutoka kundi B.

Mejdi Traore alikuwa wa kwanza kuifungia mabao Esperance katika dakika ya tisa.

Bao la pili lilipachikwa na Mkameruni Joseph Ndjeng ambaye alifanikiwa baadae kufunga mabao mengine mawili na kuhesabu mabao matatu aliyofunga peke yake.

Katika mechi za mwisho za makundi kati ya tarehe 16-18 mwezi huu wa Septemba, Ahly itakabiliana na Esperanace huku Wydad hawana budi kusafiri hadi Algeria kuikabili Mouloudia.

Klabu ya Enyimba ya Nigeria ilikuwa ya kwanza kufuzu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Soka barani Afrika walipoilaza Al Hilal ya Sudan mabao 2-1siku ya Ijumaa.