Mgogoro Libya Mapigano makali Bani Walid

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wapiganaji wa Waasi wakielekea Bani Walid

Wapiganaji saba wa waasi nchi Libya wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa kwenye mapigano makali katika mji wa Bani Walid.

Wapiganaji wanasema walisalitiwa na wakazi wa eneo hilo ambao walisema wako upande wao kisha wakawapeleka kushambuliwa.

Nato inashambulia mji huo ambao unashikiliwa na vikosi vya Gaddafi, lakini washambuliaji wanapungukiwa na nguvu ya kuuchukua, mwandishi wa BBC anasema.

Wakati huo huo walinzi 15 wameuawa wakati vikosi vya Gaddafi viliposhambulia kisima cha mafuta karibu na mji wa Ras Lanuf.

Mfanyakazi wa mafuta aliyejeruhiwa alisema msafara wa magari ulikaribia kisima hicho kinachodhibitiwa na Baraza la Mpito kuelekea katika mji Sirte na kufanya shambulio la kushtukiza.

Kiwanda hicho cha mafuta kinadhaniwa kuwa hakikuwa kinafanya kazi.

Mashambulizi hayo yametokea siku moja baada ya mtoto wa Gaddafi Saadi kupewa hifadhi nchini Niger.

Vikosi vinavyompinga Kanali Gaddafi sasa vinadhibiti sehemu kubwa ya Libya ukiwemo mji wa Tripoli. Vikosi vya Gaddafi bado vinashikilia takriban miji mitatu ikiwemo Bani Walid na Sirte.

Bado haijulikani Kanali Gaddafi yuko wapi. Alisema atafia Libya.