'Uislamu msimamo wa kati' waongoza Libya

Mkuu wa baraza la mpito la taifa NTC ametoa hotuba yake ya kwanza kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, tangu kuondolewa kwa Kanali Muammar Gaddafi.

Mustafa Abdul Jalil ameorodhesha mipango yake ya kuunda taifa la kisasa la kidemokrasia ikiwa katika misingi ya " Uislamu wenye msimamo wa kati"kwa maelfu ya watu wanaomwuunga mkono huku wakipeperusha bendera katika uwanja wa wazi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Mustafa Abdul Jalil

Awali, Kanali Gaddafi alizungumza kupitia televisheni kupambana " mpaka kupatikane ushindi".

Kanali Gaddafi mwenye umri wa miaka 69 hajulikani alipo mpaka sasa.

"Kilichobaki kwetu sisi ni kupambana mpaka tupate ushindi na kuyashinda mapinduzi," Kanali Gaddafi alinukuliwa akisema katika taarifa iliyosomwa na mtangazaji kutoka kituo cha televisheni kinachomwuunga mkono.

Licha ya utawala wa mpito kuahidi kuunda serikali ya mpito nchini Libya katika siku 10 zijazo, bado kuna changamoto kubwa katika kuleta utulivu nchini humo, alisema mwandishi wa BBC aliyopo Tripoli Peter Biles.

Majeshi yanayompinga Gaddafi sasa yanadhibiti maeneo mengi ya Libya lakini wanaomtii bado wanashikilia miji ya Sirte na Bani Walid, na kupambana vikali kuliko ilivyotegemewa.

Wakati huo huo, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty limetoa wito kwa baraza la NTC kuchukua hatua za kuzuia unyanyasaji wa binadamu unaofanywa na majeshi yanayompinga Kanali Gaddafi.