Meireles wa Chelsea aishutumu Liverpool

Mchezaji mpya aliyesajiliwa na Chelsea Raul Meireles ameishutumu klabu yake ya zamani ya Liverpool kwa kuvunja makubaliano waliyoafikiana na hatimaye kumlazimisha kuwasilisha barua ya maombi ya uhamisho.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Raul Meireles

Kiungo huyo anayechezea timu ya Taifa ya Ureno, aliondoka Anfield kwenda Stamford Bridge kwa kitita cha paundi milioni 12 siku ya mwisho kabla ya kufungwa dirisha la usajili ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu alipojiunga na Liverpool akitokea FC Porto.

Meireles amesema: "Ninachoweza kusema niliahidiwa Liverpool lakini nilichoahidiwa hakikutekelezwa."

Ameongeza kusema: "Liverpool ilinitaka niwasilishe barua ya maombi ya uhamisho, hilo ni jambo la kawaida."

Kumekuwa na uvumi ukizagaa kwamba Liverpool ilimuahidi Meireles nyongeza ya mshahara kwa asilimia 100 iwapo kiwango chake kingepanda katika msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu ya England na nyongeza hiyo hakupewa licha ya kiungo huyo kucheza mechi 35 na kufunga mabao matano.

Meireles amebainisha suala zima la kujiunga na Chelsea kwamba kamwe hakutaka kuhama Anfield na kuna siku ataeleza kwa nini alichukua hatua hiyo.

Hata hivyo hata katika mtandao wake rasmi wa Chelsea aliouzindua siku ya Jumatatu, Meireles amekataa kueleza kwa undani alichoahidiwa.