'Waliopelekwa kwa siri' Uganda waachiwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Al-Amin Kimathi

Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Kenya Al-Amin Kimathi ni miogoni mwa washukiwa watano wa shambulio la bomu la mjini Kampala wakati wa michuano ya kombe la dunia ya 2010 aliyeachiliwa na mahakama nchini Uganda.

Alikamatwa mwaka uliopita baada ya kwenda nchini Uganda kutoa ushauri kwa Wakenya waliotuhumiwa kuhusika na mashambulio hayo.

Wanaharakati wanaotetea haki za binadamu wamekuwa wakidai aachiliwe huru kwa sababu kukamatwa kwake kulifanyika kiholela.

Mashtaka dhidi yake yalifutwa.

Wengine ambao wameachiliwa ni raia mwengine wa Kenya, Msomali mmoja na raia wawili wa Uganda kwa sababu ya kukosa ushahidi.

Hata hivyo wengine 14 bado wako mbaroni.

Kundi la Al-Shabab limesema ndilo liliofanya shambulio hilo ambapo watu 76 waliuawa kwa sababu Uganda imetuma wanajeshi wake nchini Somalia.