Ugiriki yatetewa juu ya uchumi wake

George Papandreou
Image caption Rais wa Ugiriki George papandreou

Viongozi wa Ugiriki,Ufaransa na Ujerumani wamesema kuwa Ugiriki ni ''sehemu muhimu'' ya nchi zinazotumia sarafu ya euro.

Inafuatia mkutano uliofanyika kwa njia ya simu kati Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou, Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na Chansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Kuna wasiwasi kuwa Ugiriki huenda ikashindwa kulipa deni lake.

Matamshi hayo yanalenga kutuliza hali katika masoko ambayo yamekuwa na msukosuko katika majuma ya hivi karibuni kutokana na hali inayozunguka uwezo wa kifedha wa Ugiriki.

Mipango iwekwe kusaidia uchumi wa Ugiriki

Hili limeongeza wasiwasi kuwa Ugiriki huenda wakalazimika kuondoka katika muungano wa nchi 17 zinazotumia sarafu moja.

Msemaji wa serikali ya Ugiriki Elias Mossialos alisema: ''Pamoja na uvumi ulioenezwa katika siku chache zilizopita,ilisisitizwa na wote kwamba Ugiriki ni sehemu muhimu ya nchi zinazotumia sarafu ya euro.''

Bi Merkel na Bwana Sarkozy walisema katika taarifa ya pamoja: ''Kuweka mipango madhubuti ni muhimu kwa uchumi wa Ugiriki ili kusaidia uchumi wa nchi hiyo kukua.''