Denmark yampata waziri mkuu mwanamke

Helle Thorning Schmidt
Image caption Helle Thorning Schmidt

Chama cha mrengo wa kati cha Denmark kimepata ushindi katika uchaguzi mkuu, na sasa wanaondoka upande wa upinzani baada ya muongo mmoja.

Huku ikiwa kura zote zimehesabiwa, mrengo huo ukiongozwa na kiongozi wa chama cha Social Democratic Helle Thorning-Schmidt unaonekana kupata ushindi wa wingi wa wabunge.

Schmidt aahidi kuachana na sheria kali za uhamiaji

Atakuwa mwanamke wa kwanza kuwa waziri mkuu nchini Denmark. Waziri mkuu aliye madarakani Lars Lokke Rasmussen amekubali kushindwa.

Katika kampeni zake Bi Thorning-Schmidt aliahidi kuongeza kodi na matumizi ya serikali.

Pia aliahidi kufutilia mbali sheria kali ya uhamiaji iliyopendekezwa na moja ya chama kilichoko katika serikali ya mseto ya sasa.

Ikiwa karibu kura zote zimehesabiwa, mrengo wa kati umeshinda viti 89 kati ya viti 179 katika bunge la Denmark dhidi ya 86 vya mrengo wa kulia.

Rasmussen aliongoza muongo mmoja

" Tumeshinda... leo tumeweka historia," Bi Thorning-Schmidt aliwaambia wale wanaomuunga mkono.

Bwana Rasmussen amesema alimpigia simu Bi Thorning-Schmidt kumpongeza, lakini akaongeza: " Leo namkabidhi Helle Thorning-Schmidt funguo za ofisi ya waziri mkuu. Na Helle, zitunze vizuri. Kwa kuwa nimekuazima kwa muda."

Mrengo unaoongozwa na Bwana Rasmussen umekuwa kwenye uongozi kwa muongo mmoja.