Eritrea yatakiwa kuwaachia wanasiasa 11

Image caption Rais wa Eritrea Isais Afewerki

Shirika la Kutetea haki za binadamu limetoa wito kwa serikali ya Eritrea kuwaachia huru wanasiasa waandamizi na maarufu 11wanaoshikiliwa kwa miaka kumi sasa.

Wanasiasa hao wanashikiliwa bila kufunguliwa mashtaka, shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limesema.

Kundi hilo, akiwemo makamau wa rais wa zamani na mawaziri wa zamani wawili walikamatwa baada ya kutaka yawepo mageuzi ya kisiasa.

"Hatujawa na mawasiliano tangu alipokamatwa," kaka yake waziri wa zamani wa mambo ya nje Haile Woldetensae ameiambia BBC

Rais Isaias Afewerki, ambaye aliiongoza Eritrea kupata uhuru wake 1993, hana uvumilivu na kukosolewa.

Eritrea hairuhusu vyama vya upinzani, uhuru wa waandishi wa habari au mashirika ya kiraia.

Claire Beston kutoka Shirika la kutetea haki za binadamu amekiambia kipindi cha BBC Network Afrika kuwa wafungwa hao akiwemo mwanamke Aster Fissehatsion – walikuwa ‘wanasiasa waandamizi maarufu wa vita ya kuleta uhuru na wajumbe katika chama tawala.

"Mwezi Mei 2001, watu wengine wanne, walichapisha barua ya wazi wakitaka mageuzi na kuwepo kwa mazungumzo ya demokrasia, utawala na sheria na haki," alisema.

"Wakati watatu kati yao walikuwa nje ya nchi na mmoja akaachia uungaji wake mkono, waliobakia 11 walikamatwa Septemba 11, 2001, baada ye kidogo tu wakatuhumiwa kufanya uhalifu dhidi ya usalama wa taifa."

Michelle Kagari, Naibu mkurugenzi wa Amnesty barani Afrika alisema maadhimisho hayo yalikuwa ni ‘kumbukumbu ya kusikitisha kwa Rais Afewerki kutokujali haki za msingi za uhuru wa kujieleza.’

Kaka wa Haile Woldetensae Daniel alisema hakuna anayethubutu kuuliza mamlaka kuhusu aliko kaka yake kwa kuogopa kukamatwa.

"Hawajawahi kufunguliwa mashtaka, hawajawahi kupata wakili, hakuna aliewahi kuwatembelea tangu walipochukuliwa majumbani kwao saa 12 na nusu asubuhi, hawajaonekana tena," alisema.

Alimwelezea ndugu yake kama "mtenda haki na mtu wa kawaida, mpigania uhuru wa Eritrea".