Sudan mbili zakubaliana juu ya mipaka

Haki miliki ya picha
Image caption Sudan na Sudan Kusini

Sudan na Sudan Kusini wametia saini makubaliano ya kuvuka mipaka- mapatano ya mwanzo baina ya nchi hizo mbili tangu kupatikana uhuru wa kusini mwezi Julai.

Pande hizo mbili zimekubaliana kufungua mipaka 10 ili kurahisisha usafiri.

Wiki iliyopita, Sudan kusini imeishutumu kaskazini kwa kuvuruga uchumi kufuatia kuzuia mizigo kupitishwa, tangu mwezi Mei.

Kwa upande mwengine, Sudan imeishutumu kusini kwa kuchochea ghasia kwenye mipaka ya miji ya Kordofan kusini na Blue Nile, madai yaliyokanushwa na Juba.

Makubaliano hayo, yaliyotiwa saini Khartoum na kusimamiwa na mpatanishi wa Umoja wa Afrika na aliyekuwa Rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki, alisema mipaka hiyo italindwa na askari sita kutoka kila upande na askari wengi sita wa kutunza amani kutoka Ethiopia, imeeleza shirika la habari la Sudan.

Mwezi Julai, baraza la usalama la umoja wa mataifa lilitoa idhini ya kusambazwa kwa askari 300 kutoka Ethiopia ili kusimamia kuondoa majeshi kwenye eneo la amani baina ya nchi hizo mbili.

Licha ya makubaliano hayo, pande hizo mbili hazijabainisha wazi mipaka yao- hasa Abyei, linalozozaniwa na pande zote mbili.