Sudan yapiga marufuku vyama vya kisiasa

Sudan imepiga marufuku vyama vya kisiasa kutoka Sudan Kusini.

Image caption Ramani ya Sudan

Sudan imeamuru vyama vya kisiasa 17 kusitisha shughuli zao ikisema kuwa wengi wa viongozi na wanachama wanatoka taifa jipya la Sudan kwa hiyo ni wageni.

Chama cha SPLM-North ni mojawapo ya vyama vilivyopigwa marufuku na kilisimamishwa juma lililopita.

Chama hicho kina uhusiano thabiti na waliokuwa waasi kutoka kundi la SPLM ambalo sasa ni chama tawala Sudan Kusini, taifa jipya lililojitenga na Sudan Kaskazini mwezi Julai.

Hii ni baada ya mapigano kuzuka, katika baadhi ya majimbo yaliyoko mpakani, baina ya wanajeshi wanaoiunga mkono SPLM-Kaskazini na vikosi vya serikali.

Raia wa Sudan Kusini walipiga kura ya maoni Januari mwaka huu baada ya makubaliano ya amani mwaka 2005, yaliyositisha vita vya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miongo kadha na kusababisha vifo vya watu kama milioni 1.5.

Uraia

Taarifa kutoka Baraza la Masuala ya Vyama vya Kisiasa (Political Parties Affairs Council) imesema vyama vya kisiasa 17 vinachukuliwa kama 'vyama vya ng'ambo'.

"Viongozi pamoja na wanachama wa vyama hivyo wamepoteza uraia wao" imeongeza.

Vyama hivyo vina haki ya kuunda vyama vipya vikizingatia sheria zilizopo, kwa mujibu wa Shirika la habari la kiserikali la Suna.