Mtalii anashikiliwa na al-Shabaab

Kundi la al-Shabaab
Image caption Kundi la al-Shabaab

Serikali ya Somalia imesema kuwa inaamini raia huyo wa Uingereza, aliyetekwa na genge la watu waliokuwa wamebeba bunduki, anashikiliwa na kundi la wapiganaji la al-Shabaab.

Judith Tebbutt, mwenye umri wa miaka 56 alitekwa nyara, alipokuwa kwenye hoteli moja huko Kiwayu karibu na Lamu nchini Kenya.

Genge hilo lilimpiga risasi mumewe mwanamama huyo, David Tebbutt, mwenye umri wa miaka 58.

Waziri wa ulinzi nchini Somalia, Hussein Arab Issa, amesema al-Shabaab walimvusha mpaka Bi Tebbutt na kumpeleka Somalia.

Lakini serikali ya Somalia imesema kuna uwezekano kuwa anashikiliwa na makundi mengine.

Mwandishi wa BBC wa Afrika Mashariki, Will Ross, amesema kuwa serikali ya Somalia inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha anaachiwa.

Aliongeza, iwapo Bi Tebbutt anashikiliwa kwenye eneo linalodhibitiwa na al-Shabaab serikali ya Somalia itahitaji msaada kutoka nchi zingine.

Hakuna taarifa za kutosha kuhusu yaliyomsibu Bi Tebbutt baada ya kutekwa na genge hilo na kusafirishwa kwenye boti iendayo kasi.

Baada ya mshukiwa mmoja raia wa Kenya kukamatwa, inadhaniwa kuwa genge hilo linajumuisha raia wa Somalia na Kenya.

Waziri Mkuu Cameron, Jumatano, alisema " tunafanya kila lililo katika uwezo wetu katika suala hili la kusikitisha"

Ofisi ya mambo ya Nje ya Uingereza inaendelea kutoa tahadhari ya kutosafiri kilomita 30 karibu na mpaka wa Somalia.