Kesi ya Facebook yafutwa Zimbabwe

Haki miliki ya picha other

Kesi dhidi ya raia wa Zimbabwe Vikas Mavhudzi, anayeshutumiwa kwa uchochezi kutokana na taarifa inayodaiwa kuwekwa kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, imefutwa.

Waendesha mashtaka wameshindwa kupata tena ujumbe anayodaiwa kuweka kwenye ukurasa wa Waziri mkuu Morgan Tsvangirai mwezi Februari iliyosifu machafuko ya Misri.

Alikaa gerezani kwa zaidi ya mwezi mmoja kabla ya kupewa dhamana mwezi Machi 13.

Mvutano baina ya Bw Tsvangirai na Rais Robert Mugabe unaongezeka huku uchaguzi ukikaribia mwakani.

Mahasimu hao wa muda mrefu walikubali kugawana madaraka baada ya uchumi kuporomoka kufuatia uchaguzi wenye utata mwaka 2008.

Wazimbabwe wengine sita nao wamefikishwa mahakamani kwa kuchochea ghasia baada ya kuhudhuria mhadhara juu ya mapinduzi ya Misri iliyomtoa kiongozi mkongwe Hosni Mubarak.

Semina hiyo iliyofanywa na mhadhiri wa chuo kikuu iliuliza "ni lipi watu wameweza kujifunza"- ambapo waendesha mashtaka wanasema inamaanisha kwamba walikuwa wakipanga ghasia kama hizo dhidi ya Rais Mugabe, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1980.

Mwandishi wa BBC Brian Hungwe kwenye mji mkuu, Harare alisema, kesi ya Bw Mavhudzi ni ya kwanza ya aina yake katika nchi hiyo inayohusisha Facebook.