Waandamanji wauawa mjini Sanaa Yemen

Yamkini watu 26 wameuawa mjini Sanaa, nchini Yemen baada ya vikosi vya usalama kuwamiminia risasi maelfu ya waandamanji waliojitokeza kupinga utawala wa Rais Ali Abdullah Saleh.

Image caption mamia ya watu wamejeruhiwa baada ya waandamanji kushambuliwa

Maelfu ya watu walijotokeza barabarani kumshinikiza Rais Saleh ajiuzulu.

Haya ndio makabiliano mabaya zaidi kutokea nchini Yemen katika miezi ya hivi karibuni tangu raia waanze kupinga utawala wa kiongozi huyo.

Wizara ya Ulinzi, kwenye taarifa iliochapishwa kwenye wavuti wake, imedai kuwa ghasia zilizuka baada ya waandamanaji kuwarushia walinda usalama mabomu yaliotengenezwa na petroli.

Wizara hio pia imedai kuwa makundi ya waislamu ndio yalioshambulia waandamanaji hao.

Hata hivyo walioshuhudia tukio hilo wanasema maafisa wa usalama walifyetulia risasi waandamanaji hao walipokuwa wanakaribia kasri ya Rais Saleh.

Mashaidi wanasema bunduki za rashasha na ndege za kijeshi zilitumika kuwashambulia watu waliokuwa wanaandamana. Gesi za kutoa machozi pia zimetumika kuwatawanya waandamanaji hao.

Madaktari mjini Sanaa wanasema mamia ya watu wanatibiwa baada ya kupata majeraha ya risasi na kuvuta mvuke wa gesi za kutoa machozi.

Rasi Ali Abdullah Saleh kwa sasa yuko nchini Saudi Arabia ambako anapokea matibabu kufuatia majeraha alioyapata wakati kasri yake ililposhambuliwa mwezi Juni.

Taarifa zinasema kuwa viongozi wa upinzani wamepuuza pendekezo lake kuwa makamu wa rais aongoze mazungumzo ya upatanishi, wanasema hiyo ni njama ya Rais Saleh ya kuongeza muda wake mamlakani.