Arsenal yashinda, United yaua Kombe la Carling

Kieran Gibbs, Alex Oxlade-Chamberlain na Yossi Benayoun walifunga mabao yao ya kwanza kwa Arsenal baada ya timu hiyo kuwa nyuma ya bao moja na kufanikiwa kuitoa Shrewsbury katika kuwania Kombe la Carling.

Image caption Wachezaji wa Arsenal

Shrewsbury walikuwa wa kwanza kulitia msukusuko lango la Arsenal kipindi cha kwanza na alikuwa James Collins aliyefunga bao hilo kwa kichwa ambapo kabla ya hapo mkwaju wa Mark Wright uligonga mlingoti wa lango la Arsenal.

Lakini Arsenal walisawazisha kwa bao la kichwa lililofungwa na Gibbs baada ya kupokea pasi ya pembeni kutoka kwa Carl Jenkinson.

Baada ya mapumziko Oxlade-Chamberlain aliipatia Arsenal bao la pili kwa mkwaju mkali alioufumua kutoka umbali wa yadi 25 kabla ya Benayoun kuihakikishia ushindi Arsenal kwa kufunga bao la tatu.

Matokeo hayo yamekuwa ya kuliwaza kwa meneja wa Arsenal Arsene Wenger, ambaye kikosi chake kimeanza vibaya heka heka za ligi msimu huu ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoanza kuifunza klabu hiyo.

Kwa upande mwengine Michael Owen ameanza vizuri mechi yake ya kwanza msimu huu wakati timu yake ya Manchester United kufanikiwa kusonga mbele raundi ya nne ya michuano ya Kombe la Carling baada ya kuilaza Leeds nyumbani kwao mabao 3-0.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Michael Owen na Giggs

Wageni, Manchester United, licha ya kufanya mabadiliko ya wachezaji 11 waliocheza katika kikosi kilichoichapa Chelsea mwishoni mwa wiki, walicheza vizuri.

Owen alifunga bao la kuongoza baada ya kupokea pasi ya Dimitar Berbatov kabla ya kufunga bao la pili muda mfupi baadae.

Ryan Giggs alifanya ubao wa matangazo usomeke mabao 3-0 baada ya kuambaa na mpira upande wa kushoto na kuachia mkwaju safi uliokwenda moja kwa moja wavuni, bao hilo lililotosha kuihakikishia timu yake nafasi ya kusonga mbele.

Wolves nayo imefanikiwa kusonga mbele raundi ya nne ya Kombe la Carling kwa ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Millwall.

Matokeo mengine Stoke imefanikiwa kuwatoa Tottenham katika mashindano hayo baada ya kwenda sare ya kutofungana, lakini wakati wa kupigiana mikwaju ya penalti, Stoke walifanikiwa kupata mikwaju 7 dhidi ya 6 ya Tottenham.

Aston Villa wakiwa nyumbani kwao waliaga patashika za Kombe la Carling baada ya kufungwa mabao 2-0 na Bolton.

Newcastle imefanikiwa kusonga mbela baada ya kuilaza Nottingham Forest kwa mabao 4-3.

Mechi nyinge matokeo ya Kombe la Carling ni kama ifuatavyo:

Aldershot 2-1 Rochdale, Blackburn 3- 2 Leyton, Burnley 2- 1 MK Dons na Crystal Palace 2-1 Middlesbrough.