Unyakuzi ardhi Afrika

Shirika la Oxfam Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Shirika la Oxfam

Shirika la misaada la Oxfam limeonya kuwa ongezeko la mahitaji ya ununuzi ardhi linawapokonya wakulima ardhi na kuziacha jamii masikini bila makao.

Oxfam inasema hadi ekari milioni 560 zimeuzwa ama kukodishwa kote ulimwenguni tangu mwaka 2001.

Nusu ya biashara hiyo imefanyika Afrika na ardhi iliyouzwa ni sawa na nchi nzima ya Ujeremani ikiwa ni hekta milioni 35.

Jamii masikini kutoka Uganda na kusini mwa Sudan zimeathiriwa na biashara hiyo.

Taarifa hiyo pia imeangalia hali hiyo katika nchi za Honduras, Guatemala na Indonesia.

Mkuu wa shirika hilo la Oxfam Barbara Stocking amesema kuwa mashindano ya wawekezaji kunyakuwa ardhi yanapuuza mahitaji ya wale wanaoishi katika ardhi hizo na kuzitegemea kwa maisha yao ya kila siku.

Oxfam inasema kati ya walioathirika zaidi ni wanawake ambao licha ya kuzalisha 80% ya chakula katika baadhi ya nchi masikini, mara nyingi hawana uwezo mkubwa kwa kuwa sheria nyingi za ardhi haziwapi haki.

Shirika hilo linasema unyakuzi wa ardhi ulishika kasi tangu 2008 wakati bei zilipopanda na kuliweka wazi suala la upungufu wa chakula.

Oxfam limesema ongezeko la mahitaji ya chakula, pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa na kutumiwa kwa ardhi iliyokuwa awali inatumika kwa kilimo zitachagia sana kuongeza mahitaji ya uuzaji ama ukodishaji ardhi katika siku za usoni.