Obama akutana na rais wa Palestine

Rais Barack Obama wa Marekani amefanya mazungumzo ya faragha na kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas, pembezoni mwa mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

Image caption Mikutano imefanyika Gaza kuunga mkono mikakati ya Palestine

Palestina inatarajiwa kuwasilisha ombi la kuruhusiwa kuwa mwanachama wa Umoja huo hapo ijumaa.

Hukuna taarifa zozote kuhusu mkutano huo wa faragha lakini ikulu ya White House imesisitiza kuwa itapinga ombi hilo.

Rais Obama anasema kuwa Palestina wanastahili kuwa nchi huru lakini hilo litapatikana kupitia mazungumzo ya amani na wala sio azimio litakalo pitishwa na umoja wa mataifa.

"Amani inapatikana kwa bidii. Ikiwa inapatikana kupitia azimio la umoja wa mataifa basi amani mashariki ya kati ingekuwa ishapatikana zamani sana" Obama amesema.

Hotuba ya kiongozi huyo wa marekani inafuata harakati kali za kidiplomasia katika makao makuu ya umoja wa mataifa mjini New York kuhusu ombi la Palestina kuwa mwanachama.

Kwa upande wake Rais Nicholas Sarkorzy wa Ufaransa ameonya kuwa huenda ghasia zikaibuka mashariki ya kati ikiwa muafaka kuhusu suala hilo hautapatikana.

"Ni nani anaweza hoji kuwa kura ya turufu ikipigwa katika baraza la uslama haitachochea ghasia mashariki ya kati ?" amesema Sarkorzy.

Rais wa Ufaransa amependekeza kuwa Palestina ipewe uwezo zaidi katika Umoja huo licha kuwa sio mwanachama kamili wa umoja wa mataifa.

Mpatanishi mkuu wa Palestina Nabil Shaath amesema wanatofautiana na marekani kwa kuwa ni haki yao kisheria na kisiasa kuwa wanachama wa umoja huo.