Ranieri kocha mpya Inter Milan

Kocha wa zamani wa Chelsea Claudio Ranieri ametangazwa kuwa kocha mpya wa Inter Milan kwa mkataba unaokwenda hadi mwaka 2013.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kocha mpya wa Inter

Tangazo hilo limefuatia kufukuzwa kazi kwa Gian Piero Gasperini siku ya Jumatano asubuhi.

Gasperini alisimamishwa kazi baada ya kufungwa mechi nne na kutoka sare mchezo mmoja katika mechi tano ambazo alikuwa akiongoza kikosi hicho.

Gasperini alikuwa amechukua nafasi ya Leonardo mwezi Juni.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Gasperini

Hii itakuwa kazi ya kwanza kwa Ranieri tangu alipoondoka Roma mwezi Februari kutokana na kupoteza mechi nne mfululizo.

"Claudio Ranieri sasa ni kocha rasmi wa Inter," imesema taarifa ya klabu hiyo siku ya Alhamisi.

Chini ya Gasperini, Inter ilifungwa 3-1 dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu Novara, siku ya Jumanne, na kupoteza michezo dhidi ya Palermo kwenye ligi kuu, Trabzonspor katika Klabu Bingwa Ulaya, na kwa mahasimu wao AC Milan kwenye mchezo wa kombe la Italia.

Mchezo pekee katika uogozi wa Gasperini uliomalizika bila kufungwa ni sare ya 0-0 dhidi ya Roma wiki iliyopita.

Hata hivyo Ranieri ambaye aliwahi pia kuwa kocha wa Juventus amekuwa akisuasua kushida vikombe. Kombe la mwisho aliloshinda lilikuwa la Italian Cup mwaka 1996 akiwa na Fiorentina, na pia kombe la Hispania akiwa na Valencia miaka mitatu iliyofuatia.