Jaribio lingine la kumuua Nyamwasa lazimwa

Image caption Jenerali Kayumba Nyamwasa

Mamlaka ya Afrika Kusini imezima jaribio lingine la kumuua aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Rwanda Faustin Kayumba Nyamwasa, BBC imegundua.

Jenerali huyo alikimbilia uhamishoni Johannesburg mwaka jana baada ya kutofautiana na mshirika wake wa zamani Rais Paul Kagame.

Miezi michache baadaye alipigwa risasi mjini Johannesburg. Rwanda ilikanusha kuhusika na shambulio hilo ambalo alipona.

Vyanzo vilivyo karibu na Jenerali Nyamwasa vimethibitisha kuhusu mpango huo mpya. Lkini polisi wa Afika Kusini haina taarifa ya mipango hiyo.

Vyanzo vimeiambia BBC kuwa Jenerali Nyamwasa alichukuliwa kutoka nyumbani kwake Johannesburg kwa taarifafupi mwezi uliopita baada ya taarifa za kijasusi kuibua mpango huo mpya.

Iliaminika kuwa ni kuhusu pesa zilizoletwa Afrika Kusini kutoka Rwanda kwa shambulio la kutumia bunduki, kummaliza kila mmoja aliyekuwako nyumbani kwa Jenerali huyo.

Kwa mujibu wa gazeti moja la Denmark linalotoka kwenye mtandao kwa Kinyarwanda Umuvugizi, mamlaka ya Afrika Kusini ilikamatapicha, mawasiliano ya barua pepe, bunduki na vifaa vingine vinavyohusiana na harakati hizo.

Lakini mseamaji wa polisi Afrika Kusini McIntosh Polela alisema hana taarifa yoyote ya jaribio jipya la mauaji ya Jenerali huyo akiongeza kuwa, "hata kama tulikuwa nazo hatuwezi kuwaambia".

Jenerali Nyamwasa alipigwa risasi tumboni wakati akirudishwa nyumbani kwake Johannesburg mwezi Juni 2010 na akapelekwa hospitali, wakati jaribio la pili la kumuua limezimwa na majasusi wa Afika Kusini.

Kesi mbili za watu 10 wanaotuhumiwa kwa mipango ya mauaji hayo zinaendelea Afrika Kusini.

Rwanda imekanusha tuhuma za kuhusika.

Didier Rutembesa, mshauri wa kwanza katika ubalozi wa Rwanda nchini Afrika Kusini ameiambia BBC kuwa nchi yake haina sera ya kuwaua wapinzani wake.

Ametoa wito poilis na mahakama kufanya uchunguzi badala ya kushawishiwa na vyombo vya habari.

Mapema mwaka huu, Mahakama ya Kijeshi ya Rwanda ilimhukumu Jenerali Nyamwasa miaka 24 jela kwa kuhatarisha usalama wa taifa.