Rais wa OIC ataka ushahidi wa BBC

Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa - IOC Jacques Rogge ameitaka BBC kutoa ushahidi wa madai kwamba kuna majaribio ya kutaka kupanga matokeo katika mchezo wa ngumi wakati wa mashindano ya Olimpiki mwaka 2012 mjini London.

Image caption Jacques Rogge

Kipindi cha BBC Newsnight kilitoa ushahidi wa kutolewa malipo ya siri kutoka Azerbaijan kwenda kwa Chama cha Ngumi cha Dunia-WSB- ikidaiwa watathibitishiwa medali mbili za dhahabu wakati wa michezo hiyo.

Bwana Rogge amesema:"Tunachunguza kila tuhuma kwa makini sana."

Chama cha mchezo wa ngumi za Ridhaa cha Kimataifa-AIBA- kimekanusha madai hayo.

AIBA hata hivyo kimesema kinachunguza madai hayo na Rogge akaongeza: "Tutaupokea uchunguzi wa AIBA na tumeitaka BBC kutupatia ushahidi."

Tangu madai hayo yaliposambaa, Rais wa AIBA Wu Ching-kuo amekanusha madai hayo ya BBC, akisema "madai hayo ni ya uongo kabisa," ingawa akasema atachunguza.

Kwa mujibu wa taarifa ya BBC, timu ya taifa ya Azerbaijan ililipa dola milioni tisa kutoka kwa Chama cha mchezo wa ngumi cha Dunia - WSB.

Baada ya kipindi hicho kutangazwa, AIBA ilitoa taarifa iliyosema ulitolewa mkopo na WSB kutoka kwa mwekezaji wa Azerbaijani kwa misingi ya kibiashara na kwa mtazamo wa kurejeshwa kibiashara kwa mwekezaji huyo."