Rais Saleh arudi nyumbani Yemen

Rais Ali Abdallah Saleh Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rais Ali Abdallah Saleh wa Yemen

Rais Abdullah Saleh wa Yemen amerejea nyumbani kutoka Saudi Arabia miezi mitatu baada ya kunusurika jaribio la kumuua.

Televisheni ya Yemen imesema kuwa Rais Saleh amewasili katika mji mkuu wa Sanaa kwa ndege ya kibinafsi mapema alfajiri. Hakuna taarifa nyengine zaidi zilizotolewa.

Alikwenda Saudia mwezi Juni kupata matibabu baada ya shambulio la kombora katika kasri la Rais.

Rais Saleh ambaye ameshika hatamu za uwongozi kwa zaidi ya miaka 30 amekabiliwa na miezi ya maandamano kumtaka ang'atuke madarakani. Waandishi wanasema kurejea kwake huenda kukazua vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wakereketwa wamepiga kambi nje ya eneo la Sanaa lililopewa jina la Uwanja wa Mabadiliko wakimtaka aondoke madarakani.

Ghasia katika mji mkuu zimeonesha kushika kasi wakati vikosi vitiifu kwa Rais vinavyoongozwa na mwana wa Rais Saleh, Ahmed vikikabiliana na makundi ya wanajeshi walioasi ambao sasa wamejiunga na upinzani na wapiganaji wa makabila wanaowaunga mkono waandamanaji.

Zaidi ya waandamanaji 80 wengi wao bila silaha wameuawa tangu Jumapili.

Maafisa wa matibabu wanasema mtu mmoja ameuawa usiku na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati makombora yaliporushwa katika uwanja huo. Taarifa zasema watu wanne waliuawa kaskazini mwa al-Hasaba.

Waandishi huko Sanaa wameripoti kuwepo na ongezeko la silaha na milio ya risasi katika mji huo baada ya taarifa za Rais Saleh kurejea nyumbani kusambaa. Baadhi ya milio ya risasi inasemekana ilikuwa ya kusherehekea kurejea Rais Saleh.

Televisheni ya Yemeni ilionesha picha za zamani za Rais Saleh na vile vile kucheza nyimbo za kitaifa.

Ubalozi wa Yemen mjini Washington Marekani umethibitisha kurejea nyumbani Rais Saleh. Huko Sanaa, waandamanaji wanaoipinga serikali na wale wanaomuunga mkono Rais Saleh wamefanya maandamano baada ya swala ya Ijumaa.