Rais wa Zambia akubali kushindwa

Rais wa Zambia Rupiah Banda amekubali kushindwa kwake na kiongozi wa upinzani Michael Sata.

Bw Sata, aliyegombea urais mara nne, alitangazwa kuwa mshindi usiku baada ya kupata asilimia 43 ya kura zote.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rupiah Banda na Michael Sata

"Watu wa Zambia wamezungumza na lazima sote tusikilize," Bw Banda aliwaambia waandishi wa habari, huku akifuta machozi baada ya kumaliza kutoa hotuba yake.

Chama chake cha Movement for Multiparty Democracy kimeongoza Zambia kwa miaka 20.

"Nikizungumza kwa nafsi yangu na chama changu, tunakubali matokeo. Sisi ni chama cha kidemokrasia na hakuna namna nyingine yeyote ile," Bw Banda alisema.

Siku ya Alhamis, kulikuwa na ghasia eneo la kaskazini lenye migodi zilizofanywa na wanaounga mkono upinzani wakiwa hawana subra na matokeo ya Jumanne.

Matokeo hayo yalitangazwa huku majimbo saba yakiwa bado kura zao kuhesabiwa, lakini maafisa wa uchaguzi wamesema Bw Banda hatoweza kumfikia Bw Sata.

Mwandishi wa BBC Louise Redvers kwenye mji mkuu, Lusaka, alisema kuhusu tangazo hilo, wasiwasi uliogubika matokeo hayo ulisababisha makelele huku wafuasi wa Patriotic Front wakishangilia ushindi wao.

Maelfu ya watu walifurika nje ya geti lenye ulinzi mkali wakipiga ngoma, wakipiga honi na kupeperusha bendera.