Profesa Maathai akipokea tuzo ya Nobel

Profesa Wangare Maathai Haki miliki ya picha AP
Image caption Profesa Wangare Maathai

Mwanaharakati huyo wa mazingira alikabidhiwa tuzo ya Nobel mwaka 2004 huko Oslo.Wakati huo akiwa pia naibu Waziri wa Mazingira na mwanamke mwafrika wa kwanza wa kupata tuzo hiyo muhimu.

Akiwa na umri wa miaka 64 wakati huo, alitunukiwa kwa kampeini zake kuokoa miti Afrika na kuchangia katika kuleta mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ambayo yalikwenda sabamba na utunzaji mazingira.

Alielezwa kuwa ni mfano bora kwa waafrika wote waliotaka democrasia na amani.

Green belt

Alinukuliwa akisema kuwa "Amani haitopatikana bila ya kuwepo maendeleo, na maendeleo hayapatikani bila ya kuwepo usimamizi ufaao wa mazingira katika mazingira ya democrasia na amani.

"Wakati umewadia kuyatekeleza haya mabadiliko" alisema Profesa Maathai wakati akipokea tuzo yake.

Akimtambulisha wakati wa sherehe za kutoa tuzo,mwenyekiti wa kamati ya tuzo ya Nobel Ole Mjoes alisema kuwa mzozo wa Mashariki ya Kati na eneo la Darfur Sudan chanzo chake ni kung'ang'ania mali asili.

"Kulinda mazingira kumekuwa njia nyengine ya kuleta amani.....kuna uhusiano kati ya amani upande mmoja na mazingira upande mengine ambapo upungufu wa mali asili kama vile mafuta, maadini na mbao unasababisha bidhaa hizo kuzozaniwa"aliongeza mwenyekiti huyo.

Profesa Maathai alikuwa muanzilishi wa vuguvugu la Green Belt, ambalo tayari limepanda miti milioni 30 barani Afrika kukabiliana na kupotea kwa misitu na kuenea kwa jangwa.

Vuguvugu hilo pia kampeini zake zilihusu elimu,lishe bora na masuala mwengine muhimu kwa wanawake.