Meneja wa QPR asema Traore "ameaibisha"

Meneja wa Queens Park Rangers Neil Warnock amemuelezea Armand Traore kama "ametia aibu sana" baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu wakati timu yake ilipotoka sare ya kufungana bao 1-1 na Aston Villa siku ya Jumapili.

Image caption Armand Traore

Mlinzi huyo wa kushoto alioneshwa kadi ya pili ya manjano dakika za mwisho mwisho baada ya kumvaa Marc Albrighton wa Aston Villa, ingawa QPR ilifanikiwa kusawazisha bao dakika za majeruhi.

"Nilidhani alikuwa amefanya ujinga sana," alisema Warnock. "Nitampiga faini kwa kadri nitakavyoona inafaa.

"Nilimueleza kinaga ubaga, umeniangusha na umeiangusha timu."

Traore alicheza rafu hiyo kwa nia ya kumiliki mpira wakati huo QPR walikuwa wakitafuta bao la kusawazisha, lakini Warnock hakufurahishwa na kitendo alichofanya mlinzi huyo aliyemsajili hivi karibuni kutoka klabu ya Arsenal.

Meneja huyo wa QPR aliongeza: "Ukiwa mchezaji wa upande wa upinzani na umeshinda bao 1-0 ugenini, hilo ndio unalotaka kufanya. Nadhani hakutumia akili yake vizuri.

"Nilimuambia "tutakapocheza na Fulham wiki ijayo utakuwa unafanya nini? Lakini atajifunza. Ni mchezaji mzuri na atakuwa mzuri zaidi baadae."