Tevez huenda kucheza dhidi ya Bayern

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini hana budi kuamua amchezeshe Carlos Tevez katika mechi dhdi ya Bayern Munich ya Ubingwa wa Ulaya. Tevez kwa sasa muelekeo wake katika klabu hiyo unayumba.

Haki miliki ya picha elvis
Image caption Tevez na Mancini

Baada ya kwenda sare na Napoli, Man City itamkosa Mario Balotelli kwa hiyo Mancini hana budi kuchagua kati ya Tevez, Edin Dzeko na Sergio Aguero katika safu ya ushambuliaji.

Owen Hargreaves hajasajiliwa kwa michezo ya ligi ya Ulaya, kwa hiyo hataweza kuikabili timu yake ya zamani, ambayo haijafungwa katika mechi tisa zilizopita.

Mlinzi wa Bayern Holger Badstuber anaumwa mafua makali na Arjen Robben huenda asiwe tayari kuanza katika pambano hilo baada ya kucheza kwa dakika 10 baada ya zaidi ya mwezi mmoja waliposhinda mabao 3-0 dhidi ya Bayer Leverkusen mwishoni mwa wiki.

City imekwenda Ujerumani baada ya ushindi wake wa Jumamosi dhidi ya Everton, lakini watakabiliana na kikosi cha Bayern kinachoongoza msimamo wa ligi ya Ujerumani maarufu Bundesliga na haijafungwa bao katika mechi tisa ilizocheza.

Hata hivyo, David Silva amesisitiza Manchester City inaweza kushinda ugenini wakitumia mtindo wao wa ushambuliaji, ambapo hadi sasa wamefunga mabao 22 katika mechi nane.

Licha ya kuwa na kikosi imara kilichoanza vizuri msimu huu, kocha wa Bayern Jupp Heynckes amesisitiza kukabiliana na Manchester City itakuwa ni mtihani wake mkubwa wa kwanza msimu.