Tevez akanusha madai aligoma kucheza

Mshambuliaji wa Manchester City Carlos Tevez, amekanusha alikataa kucheza mechi dhidi ya Bayern Munich katika Ligi ya Ubingwa wa Ulaya.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Tevez na Mancini

Tevez alimkasirisha meneja wake Roberto Mancini kwa kuonekana hakutaka kuingia wakati wa kipindi cha pili wakati walipolazwa mabao 2-0.

Mancini alidai mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina hatacheza tena chini ya uongozi wake katika klabu hiyo ya Manchester City, lakini Tevez akajibu kwa kusema: "kila mara amekuwa akijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake."

Tevez ameongeza: "Kulikuwa na kuchanganyana katika benchi la wachezaji wa akiba na naamini nafasi yangu haikueleweka."

Akazidi kusema: "Ningependa kuomba radhi kwa mashabiki wote wa Manchester City, ambao mara zote tuekuwa na uhusiano mzuri, kwa lolote ambalo limetokea kwa kutoelewana mjini Munich.

"Wanaelewa ninapokuwa uwanjani kila mara najitahidi kuitetea klabu kwa kadri ya uwezo wangu. Kule Munich siku ya Jumanne, nilipiga jaramba kujiandaa kucheza na nilikuwa tayari kucheza.

"Huu si wakati wa kuzungumzia kwa kina nini kilichotokea. Lakini ningependa kusisitiza sikukataa kucheza.

"Nitakapotakiwa kucheza nitacheza kutimiza wajibu wangu."

Mhariri wa kitengo cha michezo cha BBC David Bond, amesema haoni kama watu hao wawili Mancini na Tevez wataonana na kuzungumza siku ya Jumatano kwa vile wachezaji wa Manchester City watakuwa katika mapumziko. City siku ya Jumamosi watakabiliana na Blackburn katika mechi ya Ligi Kuu ya England.

Mancini alikuwa anataka kumuingiza Tevez zikiwa zimesalia dakika 35 kabla mchezo haujamalizika akiwa akijaribu kurudisha mabao mawili waliyokuwa wamefungwa na Bayern.

Lakini Tevez alionekana kukataa kucheza, hali iliyomfanya Mancini kutangaza baada ya mechi: "Basi hatacheza tena chini ya uongozi wangu. Mimi na yeye tumemalizana.

"Iwapo tunataka kujiimarisha kama timu, Carlos hataichezea tena timu yetu. Kwangu mimi, basi amekwisha."

Akizungumza kupitia kitengo cha michezo cha BBC, Richard Cramer, mwanasheria wa michezo wa kampuni ya FrontRow Legal, amesema: "Kuna taratibu zilizomo ndani ya mkataba wa mchezaji, kwa kawaida kwanza ni onyo la maandishi, hatimaye onyo la mwisho la maandishi na baada ya hapo kinachofuata ni hatua ya mwisho.

"Hatufahamu iwapo Tevez atapitia hatua zozote za kinidhamu. Lakini kama ni kweli aligoma kucheza jana huo ni utovu wa nidhamu hali inayoweza kuifanya klabu ya Manchester City kumtimua."