Kiongozi wa Kiislamu 'auawa Yemen'

Mwanaharakati wa Kiislamu mwenye msimamo mkali mzaliwa wa Marekani na anayeshukiwa kuwa kiongozi wa al-Qaeda Anwar al-Awlaki ameuawa nchini Yemen, kulingana na ripoti iliyotolewa na wizara ya ulinzi.

Maafisa wa Marekani ambao majina yao hayakutajwa wamethibitisha taarifa hizo.

Awlaki, mwenye asili ya Yemen, amekuwa mafichoni huko Yemen tangu Desemba 2007.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Anwar al-Awlaki

Marekani ilimtaja kuwa "mrithi maalum wa ugaidi duniani" kwa madai ya kuhusika katika mashambulio mbalimbali na Rais wa Marekani Barack Obama inaaminiwa kwamba aliamuru binafsi mauaji yake.

Taarifa ya wizara ya ulinzi ilisema tu kuhusu kufa kwake "pamoja na washirika wake wengine".

Haijtoa taarifa zaidi za kifo chake.

Lakini vyanzo kutoka kabila moja vililiambia shirika la habari la AFP kuwa Awlaki aliuawa kwa shambulio la ndege kwenye jimbo la Marib mashariki mwa nchi hiyo, ambalo linaaminika kuwa ngome ya al-Qaeda.

Afisa huyo wa Marekani ambaye jina lake halikutajwa aliliambia shirika la habari la AP kuwa aliuliwa kwa shambulio lililofanywa na ndege ya Marekani isiyokuwa na rubani.

Hata hivyo, mwili wa kiongozi huo unasemekana kuwepo mikononi mwa nchi ya Yemen.

Kifo hicho pia kilitangazwa kwenye televisheni ya Yemen.