Liverpool yailaza Everton mabao 2-0

Andy Carroll na Luis Suarez walifanikiwa kupata mabao mawili kipindi cha pili na hatimaye Liverpool ikafanikiwa kuwalaza Everton waliokuwa wakicheza kumi katika mechi ya kusisimua na iliyojaa uamuzi wa utata.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Andy Carrol akipachika bao

Jack Rodwell alioneshwa kadi nyekundu ya utata katika dakika ya 23 katika hali ambayo mwamuzi Martin Atkinson aliona ilikuwa ni rafu mbaya wakati mchezaji huyo alipomkabili Suarez kumpokonya mpira.

Liverpool baadae walitumia nafasi hiyo kwa kushambulia kwa kasi na kufanikiwa kupata mkwaju wa penalti ambapo mkwaju wa Dirk Kuyt uliokolewa vizuri na mlinda mlango wa Everton Tim Howard.

Lakini Carroll alifanikiwa kupata bao la kuongoza kwa mkwaju wa yadi kumi na Suarez akafanikiwa kuongeza bao la pili baada ya walinzi wa Everton kuchanganyana.