Dalai Lama amefuta safari yake Afrika Kusini

Dalai Lama Haki miliki ya picha AP
Image caption Dalai Lama

Dalai Lama amefutilia mbali ziara yake ya Afrika Kusini ambapo alikuwa amealikwa na mshindi mwenzake wa tuzo ya amani ya Noble Askofu Mkuu Desmond Tutu.

Afisi ya kiongozi huyo wa kidini kutoka Tibet imesema kuwa serikali ya Afrika Kusini imekosa kumpa -Visa- kibali cha kuingia nchini humo kwa wakati. Alitarajiwa kuhudhuria sherehe za Ijumaa za kuadhimisha miaka 80 tangu kuzaliwa Askofu Tutu.

Kwa upande wake serikali ya Afrika Kusini inasema haikushinikizwa na Uchina kumzuia Dalai Lama kuizuru nchi hiyo .

Mzozo huu ulizidi kutokota pale Naibu Rais wa Afrika Kusini Kgalema Motlanthe alipofanya ziara ya siku nne nchini Uchina na kufanya mazungumzo pamoja na kutia saini mikataba kadhaa ya uhusiano wa kibiashara na uwekezaji.Hakuzungumzia suala la Visa alipokuwa Uchina.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka miwili kwa Dalai Lama kunyimwa kibali cha kuingia nchini humo.

"Muadhama Dalai Lama alikuwa asafiri tarehe 6 mwezi huu wa October lakini Visa bado haijatolewa bado" haya ni kwa mujibu wa afisi ya Dalai Lama huko India Kaskazini.

Katika taarifa iliyotolewa , Muadhama Dalai Lama amesema ameifuta ziara yake kwa kuwa hakutaka kusababisha usumbufu kwa yeyote yule, iwe ni watu binafsi ama serikali na kuwa anasikitika kutokana na usumbufu ambao umewakabili wenyeji wake na watu wengi waliomtarajia Afrika Kusini.

Uchina inamchukuwa Dalai Lama kuwa mtu hatari ambaye anachochea na kuongoza fikra za kuitenga Tibet kutoka utawala wa Uchina.

Lakini Dalai Lama amekuwa akikariri kuwa lengo lake ni kuitaka Tibet ipate uwezo zaidi wa kuendesha mambo yake binafsi lakini sio kujitawala moja kwa moja.

Maandamano yamefanywa nje ya bunge la Afrika Kusini na wanaomuunga mkono ambao wanasema uhuru wa nchi hiyo wa kujitawala na kufanya mambo yake bila ushawishi kutoka nje sasa umetiwa dosari.

Afisi ya Askofu Mkuu Tutu iliishutumu serikali ya Afrika Kusini kwa kujivuta katika suala zima la kutoa hiyo Visa.

Mwishoni mwa wiki, kituo cha amani cha Desmond Tutu kiliwasilisha malalamishi kikimtaka Dalai Lama aruhusiwe kuingia nchini Afrika Kusini.

Waliotia saini malalamishi hayo wanasema kuwa wameona aibu na vile vile kuudhika na suala zima la kucheleweshwa Visa hiyo na kuwa wanaamini Dalai Lama alikuwa ananyimwa kibali kwa kuingia nchini humo kutokana na sababu za kisiasa ambazo haziambatani na katiba ya nchi.