Mfumo mpya wa kulisaka LRA waundwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mpiganaji wa LRA

Mfumo mpya wa mawasiliano ya redio umeundwa ili kujaribu kupambana na kundi la waasi ambalo mashambulio yao yameenea maeneo mbalimbali Afrika ya kati.

Ukiwa umefadhiliwa na mashirika ya kimarekani, mfumo huo utaruhusu jamii za vijijini kupeana tahadhari.

Mpaka sasa mwaka huu takriban raia 140 wameuawa na zaidi ya 600 wametekwa na kundi la Lord's Resistance Army.

Matukio yote yataonyeshwa kwenye wavuti wa kufuatilia nyendo za LRA ambao unaweza pia kutumiwa na majeshi ya Congo na Uganda yanayopigana na waasi.

Adam Fink wa shirika la hisani lenye makao yake makuu Marekani Invisible Children, linalosaidia kufadhili harakati hizo, ameiambia BBC, "Kupitia mfululizo wa redio zenye masafa marefu, jamii zinaweza kuungana na kuwasiliana, kuambizana kundi hili linaenda wapi, kuweza kutangaza ripoti za usalama, halafu kuweza kujilinda kutokana na mashambulio ya LRA."

Kulingana na shirika la hisani lenye makao makuu San Diego, kifaa hicho kilitengenezwa baada ya mauaji ya Desemba 2009, ambapo raia 321 waliuliwa na LRA mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Licha ya ukubwa na ukatili wa "mauaji ya Makombo", jumuiya ya kimataifa haikufahamu kuhusu tukio hilo mpaka Machi 2010- miezi mitatu baadae.