Magavana wa zamani wakamatwa Nigeria

Image caption Wanasiasa wameshtakiwa na EFCC

Shirika la kukabiliana na ufisadi nchini Nigeria limewakamata magavana watatu wa zamani kwa madai ya ubadhirifu wa dola milioni 674.

Tume ya kukabiliana na makosa ya kiuchumi (EFCC) inasema kuwa waliokuwa magavana wa majimbo ya Ogun, Oyo na Nasarawa wanakabiliwa na mashtaka mazito.

Wanatarajiwa kufikishwa mahakamani katika siku chache zijazo.

Waandishi wanasema kuwa tume hiyo ya EFCC imewahi kuwakamata viongozi wakubwa katika siku za nyuma lakini imeshindwa kuwa na ushahidi wa kutosha dhidi yao.

'Walikiuka utaratibu wa kutoa kandarasi za serikali' Gavana wa zamani wa jimbo la Ogun Olugbenga Daniel, Adebayo Alao-Akala wa jimbo la Oyo na Aliyu Akwe Doma wa jimbo la Nasarawa walikamatwa siku ya Alhamisi, msemaji wa EFCC Femi Babafemi alisema.

Wakati walipokuwa kwenye uongozi, watu hao walishutumiwa kwa kutumia vibaya mamlaka katika utoaji wa kandarasi za serikali ya jimbo pamoja na kutumia pesa hizo kwa masuala yao binafsi.