AU yakana 'propaganda' za Somalia

Haki miliki ya picha reuters
Image caption Al-Shabab

Umoja wa Afrika umekataa kwamba miili ya watu 70 iliyoonyeshwa na wapiganaji wa Kisomali wa kundi la al-Shabab ni askari wa umoja huo waliouawa kwenye mapigano.

Al-Shabab iliwaonyesha waandishi wa habari miili hiyo, wakidai askari wa Burundi waliuawa Mogadishu siku ya Alhamisi.

Msemaji wa Umoja wa Afrika AU amekana madai hayo na kusema ni propaganda na kusema askari wake 10 wameuawa na wawili hawajulikani walipo.

AU ina askari 9,000 Somalia kuiunga mkono serikali dhaifu ya nchi hiyo.

Mwezi Agosti, al-Shabab ilitangaza " kujiondoa kimkakati" kutoka Mogadishu, lakini mapigano yameendelea na mabomu mawili yamelipuka katika mji huo mwezi huu.

Al-Shabab liliwaonyesha waandishi wa habari miili hiyo nje ya mji mkuu huo.

Limesema wote walikuwa wanajeshi wa kutunza amani wa Burundi.

Msemaji wa AU alisema al-Shabab imewavalisha sare askari wao wenyewe waliokufa.

Mwandishi wa BBC wa Afrika Mashariki Will Ross alisema muda mrefu, AU imekuwa ikisita kukiri kupoteza askari wengi.

Al-Shabab imedhoofika lakini mapigano ya kuudhibiti kikamilifu mji wa Mogadishu na mabomu ya hivi karibuni yanaonyesha mji mkuu huo una safari ndefu mpaka uwe tulivu, alisema.