Salva Kiir amzuru el-Bashir

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amewasili Sudan kwa ziara yake ya kwanza tangu eneo lake kujipatia uhuru mwezi wa July.

Atakutana na Rais Omar el Bashir na watakuwa na mazungumzo ya maswala mazito baina yao, wakati uhusiano baina ya Sudan na Sudan Kusini siyo mzuri.

Sudan imeishutumu Sudan Kusini kuwa inawasaidia wapiganaji katika mizozo mipya kwenye majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile.

Na Juba inaamini Khartoum piya imeyasaidia makundi kadha ya wapiganaji katika ardhi yake.

Nchi zote mbili zinakana shutuma hizo.

Bila ya shaka mazungumzo kuhusu usalama yatakuwa makali.

Wizara ya Mashauri ya Nchi za Nje ya Sudan inasema maswala mengine yatayojadiliwa ni kuhusu mipaka, ambayo bado haikupata ufumbuzi; uchumi pamoja na swala la mafuta; na mpaka wa jimbo la Abyei, lilioko kwenye mpaka baina ya nchi mbili hizo.

Sudan Kusini bado inasafirisha mafuta yake kwa kutumia mabomba yanayopita katika ardhi na bandari ya Sudan, na bado hakuna makubaliano ya jinsi ya kulipia hayo.

Maswala ya kuzungumzwa ni mazito, na imani kati ya majirani hao ni haba.

Kwa hivo ziara hii ya Rais Salva Kiir huenda ikawa hatua ya kwanza tu kabla ya kufikia makubaliano.