Mafuta yamwagika pwani New Zealand

Shughuli zinaendelea New Zealand kujaribu kuzoa tani 2000 za mafuta kutoka meli iliyobeba makontena, iliyopanda mwamba nje ya mwambao wa kupendeza wa nchi hiyo.

Haki miliki ya picha AP

Kuna wasiwasi kuwa meli hiyo, iitwayo Rena, inaweza kupasuka katika upepo mkali unaotarajiwa kesho.

Meli hiyo imekuwa ikivuja mafuta tangu ilipokwenda mrama siku ya Jumatano.

Meli sita ziko katika eneo hilo kujaribu kuyazoa mafuta hayo, lakini juhudi za kuyayusha mchirizi wa mafuta hazikufanikiwa, na viumbe katika bahari vimeanza kuathirika.

Waziri Mkuu wa New Zeland, John Key amezuru eneo hilo; na aliiambia redio ya taifa kwamba ni muhimu kuchunguza sababu ya ajali hiyo:

"Watu wanaujua mwamba huo, na kwa meli kuelekea kwenye mwamba bila ya sababu, usiku, bahari ikiwa shuari, inaashiria kuwa kuna kosa kubwa lilotokea.

Na tunahitaji kujua sababu."